Yanga inaweza kutinga robo fainali-Nabi

KOCHA MKuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema timu hiyo ina uwezo wa kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, endapo itautumia muda huu kujipanga vizuri kwa ajili ya mechi zijazo za makundi.
Akizungumza na SpotiLeo, kocha huyo amejigamba kuwa timu ilizopangwa nazo Yanga kwenye kundi D anajua uwezo na mafanikio yao huko nyuma lakini siyo kikwazo cha kuizuia klabu hiyo ya Jangwani isiende robo fainali.

“Kitu cha msingi hapa ni kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunavuka hatua hii ya makundi na kucheza robo fainali sababu uwezo huo tunao,” amesema Nabi.
Amesema anajua ugumu wa hatua hiyo hivyo wanachotakiwa kufanya ni mazoezi ya mbinu zaidi na kuutumia vyema uwanja wa nyumbani kuchukua pointi zote tisa.
Yanga imepangwa kundi D katika hatua ya makundi Kombe la Shirikisho pamoja na AS Real Bamako ya Mali, US Monastir ya Tunisia na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.