Mastaa

Faiza Ally:Diamond hajazaliwa kutatua matatizo ya watu

DAR ES SALAAM:MWANAMITINDO na mfanyabiashara Faiza Ally ameweka wazi msimamo wake kuhusu matarajio ya jamii kwa msanii maarufu Naseeb Abdul maarufu kama Diamond Platnumz, akisisitiza kuwa msanii huyo hajaja duniani kwa ajili ya kutatua matatizo ya watu wengine.

Faiza ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, ambapo ameeleza kuwa msaada wowote unaotolewa na Diamond unatokana na hiari yake binafsi na si wajibu.

“Nawakumbusha tu Watanzania, Nasib Abdul hajaja duniani kutatua matatizo ya watu. Na akifanya msaada ni kwa sababu amependa na ametaka, si lazima,” ameandika Faiza.

Ameongeza kuwa Diamond ana maisha yake binafsi na haishi kwa ajili ya kuwahudumia watu, akibainisha kuwa kama asingekuwa na uwezo au mafanikio aliyonayo leo, asingelaumiwa kwa chochote.

Faiza Ally pia amesema kuwa watu wengi wanaomsogelea Diamond, iwe ni kwa kazi au mahusiano mengine, hufanya hivyo wakiwa wanajua wazi uwezo, nguvu na nafasi aliyonayo katika jamii na kwenye tasnia ya muziki.

“Hizo ni biashara zake, nguvu zake na uwezo wake ndio uliowaleta watu wengi karibu naye. Sasa ikitokea baada ya kazi au ushirikiano kukawa na changamoto, si jukumu lake kutatua kila tatizo linalomkumba aliyefanya naye kazi,” ameandika.

Amehitimisha ujumbe wake, Faiza ametoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwafundisha watoto wao misingi ya maisha, akisisitiza kuwa msaada si haki na mtu anaponyimwa msaada hapaswi kulalamika.

“Tuwakumbushe watoto wetu kuwa msaada si haki; ukinyimwa usilalamike,” ameandika Faiza Ally, akijitambulisha kama muongeaji wa kujitolea.

Related Articles

Back to top button