Muziki

Rose Muhando alalamikia hakimiliki

Aiomba serikali ichukue hatua

DAR ES SALAAM:MALKIA wa muziki wa Injili nchini Tanzania, Rose Muhando, ameiomba Serikali kuingilia kati kwa haraka mgogoro wa hakimiliki unaomhusu, akimtaja moja kwa moja Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ili kuhakikisha anapata haki yake ya mapato kutokana na kazi zake za muziki.

Kupitia taarifa yake, ukurasa wa istagramu Rose Muhando ametoa malalamiko mazito kuhusu kile alichokitaja kuwa ni kudhulumiwa haki zake za mapato katika majukwaa ya kidijitali, akisema kwa takribani miaka 15 amekuwa akivumilia kimya kimya kwa matumaini kuwa haki ingetendeka.

Amesema maumivu na changamoto alizopitia kwa kipindi chote hicho zimemfanya sasa kuamua kufungua mdomo na kusema hadharani, ili kulinda jasho lake na mustakabali wa wasanii wengine.

Rose Muhando ameeleza kuwa chanzo cha changamoto hiyo ni ushirikiano wake wa zamani na kampuni ya Sony Music Africa, akidai kuwa licha ya kuachana na kampuni hiyo muda mrefu uliopita, bado kampuni hiyo inashikilia zaidi ya kazi zake 37 na kukataa kuziachia.

Ameongeza kuwa cha kusikitisha zaidi ni kwamba hapati hata shilingi moja kutokana na kazi hizo, ilhali ni kazi alizozitolea nguvu, muda na maisha yake yote ya kisanii.

Aidha, Rose Muhando amebainisha kuwa Serikali kupitia COSOTA (Copyright Society of Tanzania) imekuwa ikijitahidi kumsaidia kusimamia haki yake, lakini juhudi hizo zimekwama kutokana na kukosa ushirikiano kutoka kwa mwakilishi wa kampuni hiyo, Seven Mosha, ambaye amekuwa akiitwa mara kadhaa bila kujitokeza au kutoa ushirikiano unaohitajika.

Kwa mujibu wa msanii huyo, hali hiyo imemuumiza sana, imemvunja moyo na kurejesha nyuma ndoto za wasanii wengi ambao wanaendelea kudhulumiwa haki zao kimyakimya katika tasnia ya muziki.

“Kwa unyenyekevu mkubwa, Rose Muhando ameiomba Serikali kuingilia kati suala hilo kwa haraka, akimuomba moja kwa moja Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Paul Makonda, kuhakikisha haki inatendeka na haki za wasanii zinalindwa ipasavyo.”ameandika Rose Muhando

 

Related Articles

Back to top button