Muziki

Bongo Star Search msimu wa 16 kuanza rasmi Februari 7

DAR ES SALAAM:MASHINDANO makubwa ya kusaka vipaji nchini, Bongo Star Search (BSS) Msimu wa 16, yanatarajiwa kuanza rasmi Februari 7 na 8, 2026 katika Ukumbi wa La Kairo Hotel, jijini Mwanza, baada ya kuahirishwa kwa muda.

Akizungumza na waandishi wa habari Januari 9, 2027, Mkurugenzi wa Bench Mack, Madam Rita Paulsen, amesema mashindano hayo yalisitishwa awali ili kuwapa nafasi waandaji kujipanga vizuri zaidi na kuja na ubunifu mpana kwa ajili ya Watanzania.

Amesema msimu huu utakuwa wa kipekee kwani mbali na uimbaji, wameongeza vipaji vingine vikiwemo uchezaji, uchekeshaji (comedy), uigizaji, sarakasi na uchoraji, tofauti na misimu ya awali iliyojikita zaidi kwenye waimbaji pekee.

“Kwa msimu huu, mshiriki anatakiwa awe na kipaji, kujiamini, mwonekano wa kistaa na kupendeza. Baada ya kuwa na sifa hizo, ajitokeze kwenye usahili na kuonesha kipaji chake,” amesema Paulsen.

Ameongeza kuwa usahili wa vipaji vyote utafanyika kwa wakati mmoja, na hata wale waliowahi kushiriki misimu ya nyuma bila kushinda wanakaribishwa kushiriki tena.

Ratiba ya usahili ni kama ifuatavyo: Februari 7–8, 2026 – Mwanza (La Kairo Hotel), Februari 14–15 – Arusha (SGR Resort), Februari 21–22 – Mbeya (GR Hotel), Machi 7–8 – Nairobi, Machi 13, 14 na 15 – Dar es Salaam (Makumbusho ya Taifa), Machi 28 hadi Aprili 1 – Dodoma (Royal Virage).

Amesema usahili utafanyika kuanzia asubuhi hadi kukamilika kwa washiriki wote. Kuhusu usahili wa mtandaoni, Paulsen amesema waombaji watapewa maelekezo maalum ambapo majaji watapitia kazi zao, na wale watakaofaulu watawasiliana nao ili kufika Tanzania kuendelea na mashindano.

Amefafanua kuwa kutakuwa na majaji tofauti kulingana na aina ya vipaji, na hatimaye washiriki 15 bora watachaguliwa kuingia hatua za juu za mashindano.

Kwa upande wa uzinduzi, amesema uzinduzi wa Bongo Star Search Msimu wa 16 utafanyika Nairobi Machi 12, 2026, ikiwa ni mara ya kwanza uzinduzi huo kufanyika nje ya Tanzania baada ya uzinduzi uliofanyika Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Chanel ya Sinema Zetu ya Azam, Sophia Mgaza, amesema vipindi vya Bongo Star Search vitarushwa kila Jumapili saa tatu usiku kupitia Chanel ya Sinema Zetu, huku kipindi cha kwanza kikianza rasmi Machi 22, 2026 saa mbili kamili.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button