Prince Dube mchezaji bora wa Yanga mwezi Desemba

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Prince Dube, ameibuka mchezaji bora wa klabu hiyo kwa mwezi Desemba, tuzo inayodhaminiwa na NIC Insurance, baada ya kuonesha kiwango bora na mchango mkubwa katika michuano ya Ligi Kuu na Ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Dube alichaguliwa kufuatia mwendelezo wa kiwango chake kizuri cha ufungaji, kujituma uwanjani na mchango wake katika ushindi mbalimbali uliopatikana na Yanga ndani ya mwezi huo, hali iliyomfanya kuwavutia kamati ya tuzo hiyo.
Kwa mujibu wa uongozi wa klabu, tuzo hiyo ni utaratibu wa kawaida wa Yanga SC wa kumtambua na kumuenzi mchezaji aliyefanya vizuri zaidi kila mwezi, ikiwa ni sehemu ya motisha kwa wachezaji kuendelea kuongeza bidii na ushindani wa ndani.
Kupitia tuzo hiyo, Dube ameendelea kudhihirisha umuhimu wake ndani ya kikosi cha Yanga, akionekana kuwa mmoja wa wachezaji tegemeo katika safu ya ushambuliaji wa timu hiyo inayopigania mafanikio ya ndani na nje ya nchi.
Tuzo ya NIC Insurance Player of the Month ni sehemu ya ushirikiano kati ya Yanga SC na mdhamini wake huyo, unaolenga kukuza vipaji, kuongeza morali ya wachezaji na kuinua ushindani ndani ya klabu.




