Muziki

Inspector Haroun aachia nyimbo mbili mpya

Asema bado ana hamu na nguvu ya kuendelea na muziki

DAR ES SALAAM:MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Haroun Rashidi maarufu kama ‘Inspector Haroun Babu’, ameendelea kudhihirisha uimara wake katika tasnia ya muziki baada ya kuachia nyimbo mbili mpya zenye majina “AI” na “Maisha Ndo Haya Haya.”

Inspector Haroun Babu ameeleza kuwa wimbo wa “AI” ameutoa kwa mfumo wa audio pekee, huku wimbo wa “Maisha Ndo Haya Haya” akiutoa audio na video.

Akizungumza na Spoti Leo jijini Dar es Salaam, Inspector Haroun Babu amesema kazi zote alizoachia ndani ya kipindi cha wiki mbili zilizopita hazikushirikisha msanii mwingine yeyote, akisisitiza kuwa amezifanya peke yake kuanzia mwanzo hadi mwisho.

“Kazi nilizoachia wiki hizi mbili sijamshirikisha mtu yeyote, nimefanya mimi kama mimi,” amesema Inspector Haroun Babu.

Aidha, ameongeza kuwa video ya wimbo “AI” ipo katika hatua za maandalizi, akibainisha kuwa itakuwa tofauti kwa kuwa itahusisha matumizi ya teknolojia ya Artificial Intelligence (AI) kwa kiwango kikubwa.

Kwa kuachia kazi hizo mpya, Inspector Haroun Babu amesema bado ana hamu na nguvu ya kuendelea kufanya muziki, akiamini bado ana mengi ya kutoa kwa mashabiki wake.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button