Msuva: Kuna kitu kitatokea dhidi ya Nigeria

RABAT: WINGA wa Taifa Stars, Simon Msuva, ameibua matumaini kwa Watanzania kuelekea mchezo wa kwanza wa Kundi C wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) leo usiku dhidi ya Nigeria, akisisitiza kuwa pamoja na ukubwa wa mpinzani, kuna kitu kizuri kitatokea.
Akizungumza kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa saa 2:30 usiku kwenye Uwanja wa Fez, Morocco, Msuva alisema Stars imefika kwenye mashindano hayo ikiwa na malengo ya kweli na uzoefu wa kutosha kupambana na timu kubwa barani Afrika.
“Tuko hapa kwa ajili ya mashindano. Tunajua Nigeria ni timu kubwa na mechi haitakuwa rahisi, lakini hii ni mara ya tatu tunashiriki fainali hizi. Tumepata uzoefu, na naamini kwa uzoefu tulionao, kuna kitu kitatokea ambacho Watanzania watakipenda,” alisema Msuva.
Kwa upande wake, Charles M’mbombwa alisema kikosi cha Stars kipo tayari kushindana na kushinda, akibainisha kuwa katika soka lolote linawezekana licha ya kukutana na mpinzani mwenye historia na hadhi kubwa.
“Tuko tayari. Tunajua tunacheza na timu kubwa, lakini tumejiandaa kupambana. Kwenye soka chochote kinawezekana,” alisema M’mbombwa kwa kujiamini.
Kihistoria, Tanzania na Nigeria zimewahi kukutana kwenye fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980, ambapo Stars ilipoteza kwa mabao 3-1. Hata hivyo, safari ya sasa inaonekana kuwa na sura tofauti, huku Stars ikitafuta kuandika historia mpya mbele ya vigogo hao wa soka la Afrika.
Stars itaingia uwanjani ikitambua uzito wa mchezo huo wa ufunguzi wa kundi, lakini pia ikibeba matumaini ya Watanzania wanaotamani kuona matokeo chanya na ushindani wa hali ya juu.



