Ligi Ya Wanawake

Yanga Princess yapanda mlima kwa kasi

DAR ES SALAAM: MSIMAMO wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania umebadilika kwa kasi baada ya mechi za jana, huku Yanga Princess ikiibuka kinara mpya wa ligi baada ya ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Geita Queens.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kupanda hadi nafasi ya kwanza kwa pointi 12, ikitimiza ushindi wa mechi zote nne ilizocheza hadi sasa, na kuendelea kuonesha ubora wake msimu huu.

Kwa upande wa JKT Queens, sare ya bao 1-1 waliyolazimishwa na Fountain Gate Queens ugenini imewagarimu uongozi wa ligi, na sasa wameshuka hadi nafasi ya tatu wakiwa na pointi 10.

Simba Queens nayo imeendelea kusalia kwenye ushindani mkali wa ubingwa baada ya kupata ushindi muhimu wa ugenini wa bao 1-0 dhidi ya Ceasiaa Queens.

Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 12 sawa na Yanga, lakini ikipewa nafasi ya pili kutokana na tofauti ndogo ya mabao, Yanga ikiwa imefunga mabao 15 dhidi ya 11 ya Simba.

Matokeo haya yanaashiria mwanzo wa ushindani mkali wa mapema katika Ligi Kuu ya Wanawake, huku Yanga na Simba zikionekana kuanza kujitenga kileleni, wakati JKT Queens ikilazimika kuongeza kasi ili kurejea kwenye mbio za ubingwa.

Kadri ligi inavyoendelea, kila pointi inaendelea kuwa ya thamani kubwa, na ushindani wa nafasi za juu unaonekana kuwa mkali zaidi kuliko misimu iliyopita.

Related Articles

Back to top button