AFCON

Kakuta akutana na zali DRC

KINSHASA: TIMU ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imemuita kikosini kiungo Gael Kakuta kuchukua nafasi ya Mario Stroeykens aliyeondolewa kwenye kikosi cha Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kutokana na jeraha.

Kakuta mwenye umri wa miaka 34, aliyewahi kutambulika kama kipaji kikubwa alipokuwa kijana katika klabu ya Chelsea, kwa sasa anacheza soka la klabu daraja la pili nchini Uturuki. Hajaitumikia DR Congo kwa zaidi ya miezi 15, lakini amepata mwaliko wa kushtukiza baada ya Stroeykens kuumia goti akiwa na Anderlecht kwenye ligi ya Ubelgiji mwishoni mwa wiki.

Mchezaji huyo aliyezaliwa nchini Ufaransa atashiriki AFCON yake ya pili, huku DR Congo wakiwekwa Kundi D pamoja na Benin, Botswana na vigogo Senegal.

Kakuta alikuwa sehemu ya kikosi cha DR Congo katika fainali zilizopita nchini Ivory Coast, ambapo timu hiyo ilimaliza nafasi ya nne baada ya kupoteza dhidi ya Afrika Kusini katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu.

Licha ya kuiwakilisha Ufaransa kuanzia timu za vijana hadi chini ya miaka 21, Kakuta alichagua kuchezea DR Congo mwaka 2017.

Historia yake ya soka inajumuisha sakata maarufu la uhamisho wa Chelsea mwaka 2009, ambapo klabu hiyo ilipigwa marufuku ya usajili na FIFA baada ya kumsajili kutoka Racing Lens ya Ufaransa. Adhabu hiyo iliondolewa baadaye kufuatia uamuzi kwamba Kakuta hakuwa na mkataba halali na Lens wakati wa kusajiliwa.

Kakuta alikaa Chelsea kwa miaka minane kabla ya kuondoka mwaka 2015, lakini alicheza mechi sita pekee za kikosi cha kwanza. Alitumika kwa mikopo sita tofauti kabla ya kujiunga na Sevilla, ambako alidumu kwa msimu mmoja tu.

Kwa ujumla, Kakuta amekuwa na safari ndefu na isiyotulia, akichezea klabu 27 tofauti katika taaluma yake, huku klabu yake ya sasa ikiwa Sakaryspor ya Uturuki.

Related Articles

Back to top button