Makonda kuongoza kambi ya Taifa Stars AFCON Morocco

CAIRO: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, atakuwa sehemu ya viongozi wa kambi ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itakayokuwa nchini Morocco katika maandalizi na ushiriki wa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayoanza Desemba 21 mwaka huu.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na Taifa Stars kuhakikisha timu inapata mazingira bora ya ushindani.
Profesa Kabudi amesema hayo leo Desemba 18 wakati akitembelea kambi ya Taifa Stars jijini Cairo, Misri, akiwa ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Katika ziara hiyo, amewahimiza wachezaji na benchi la ufundi kuweka mbele uzalendo, nidhamu na mshikamano, akisisitiza umuhimu wa kuwakilisha vyema taifa katika jukwaa la kimataifa.
Ikumbukwe kuwa Taifa Stars imepangwa katika Kundi C pamoja na timu za Nigeria, Tunisia na Morocco, ambapo itaianza michuano hiyo kwa kuikabili Nigeria, moja ya timu bora barani Afrika, katika pambano linalotarajiwa kuwa gumu na la ushindani mkubwa.



