Kwingineko

Sakata la Mo Salah lachukua sura mpya, mashabiki wasimama na Slot

MILAN: MASHABIKI wa Liverpool wameweka wazi upande wanaounga mkono katika kile kinachoonekana kama mvutano unaoendelea kati ya nyota wa klabu hiyo, Mohamed Salah, na kocha Arne Slot.

Zaidi ya mashabiki 5,000 waliosafiri na timu hiyo kwenda nchini Italia waliimba kwa nguvu jina la Slot kabla na baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Inter Milan kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya jana usiku, ikiwa ni ishara isiyo na utata kuwa wamesimama na kocha wao mpya.

Slot alimuacha Salah nje ya kikosi kilichosafiri kwenda Milan, hatua iliyokuja baada ya mshambuliaji huyo kumshutumu hadharani mwishoni mwa wiki kwa kile alichokitaja kuwa ‘kutupwa chini ya basi’ na kutokuwa na uhusiano wowote mzuri na kocha huyo.

“Kusema kweli, hiyo ina maana kubwa kwangu, Lakini siyo kuhusu mimi, ni kuhusu timu. Mashabiki walikuja kwa wingi, katika kipindi kigumu kwa klabu, na tena wameonesha kuwa tunapopitia wakati mgumu, tunasimama pamoja.” – Slot alisema kuhusu sapoti ya mashabiki.

Salah, mmoja wa wachezaji wakubwa katika historia ya Liverpool, ametwaa mataji mawili ya Premier League, Ligi ya Mabingwa Ulaya na tuzo kibao za mchezaji bora. Msimu uliopita aliibuka tena mchezaji bora wa klabu baada ya kufunga magoli 34.

Lakini wiki hii imekuwa ya sintofahamu. Baada ya kukaa benchi mechi tatu mfululizo, Salah alilalamika wazi kuwa anahisi kuachwa na klabu, akidai hana uhusiano wowote na Slot. Hatimaye Jumanne mchana, alichapisha picha akiwa gym peke yake kwenye kituo cha mazoezi cha Liverpool, ikionekana kama ujumbe wa ‘nafanya kazi yangu.’

Slot, kabla ya mchezo, alisema hana uhakika kama Salah atacheza tena chini yake, na baada ya ushindi dhidi ya Inter alikwepa maswali zaidi kuhusu mustakabali wa mchezaji huyo.

“Leo ni kuhusu waliopo hapa. Katika historia tajiri ya Liverpool, kumekuwa na usiku mwingi kama huu. Lakini katika msimu ambao tumo, kupata ushindi ugenini dhidi ya timu kubwa namna hii, hilo ndilo linafaa kusikika. Nafahamu Ijumaa nitajibu maswali mengi kuhusu mambo mengine, lakini leo ni kuhusu waliopambana uwanjani.”

Related Articles

Back to top button