Jonathan Budju kufunga mwaka na wimbo mpya Ituri amani

KINSHASA: MSANII nyota wa Injili kutoka Canada, Jonathan Budju, ametangaza kuachia wimbo mpya unaolenga kuhamasisha amani katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Budju, ambaye amejipatia umaarufu mkubwa kupitia kazi zake za Injili na shughuli za kijamii kupitia taasisi yake ya JB Foundation inayofanya kazi katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, amesema wimbo huo utatolewa Desemba 19.
Akizungumza na SpotiLEO, Jonathan amesema wimbo huo aliouandaa kwa ushirikiano na waimbaji wa Ituri Gospel Artists—utaitwa “Ituri Amani.”
“Lengo letu ni kuendelea kuhamasisha amani katika maeneo ya Ituri na Kivu, mashariki mwa DRC. Ninaamini wimbo huu utawagusa wengi na kubadilisha maisha yao,” amesema Jonathan
Ameongeza kuwa atatoa video na audio kwa pamoja kupitia majukwaa yake yote ya muziki, akiamini kuwa sanaa inaweza kuwa daraja muhimu katika kuleta maridhiano na matumaini katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro.




