‘Staa’ wa filamu za mapigano wa Japan afariki

TOKYO: CARY-Hiroyuki Tagawa, mmoja wa waigizaji waliotamba kwa zaidi ya miongo minne katika filamu za mapigano, amefariki dunia akiwa na miaka 75 kutokana na matatizo yaliyotokana na kiharusi. Tagawa amefariki jana Desemba 05 huko Santa Barbara akiwa amezungukwa na familia yake, kwa mujibu wa taarifa ya mwakilishi wake.
–
Tagawa, ambaye wengi wanamkumbuka kama mchawi(adui) Shang Tsung kwenye filamu ya Mortal Kombat, alianza kutambulika kimataifa baada ya kugunduliwa na mwongozaji Bernardo Bertolucci na kupewa nafasi kwenye filamu The Last Emperor mwaka 1987. Kuanzia hapo, aliendelea kuigiza zaidi ya filamu 30, akijijengea jina kama mhusika mwerevu na mwenye ukatili wa hali ya juu sana, aina ya uhalifu uliomfanya kuwa kipenzi cha Hollywood.
–
Licha ya sura yake ya “kijambazi” kwenye skrini, nyuma ya pazia Tagawa alikuwa mtu mpole, mwenye haiba na aliyependa kuwasaidia vijana waliokuwa wanaanza filamu na sanaa za mapigano.
–
Tagawa ameacha watoto wake Calen, Byrnne na Cana, pamoja na wajukuu wake River na Thea Clayton. Hisia za upendo na heshima kwake zimeendelea kumiminika kutoka kwa watu aliowahi kufanya nao kazi na mashabiki wake duniani kote.




