Wabunifu wa mitindo kuchuana Swahili Fashion Ijumaa

DAR ES SALAAM: TAMASHA la Swahili Fashion Week (SFW) linarejea kwa msimu wake wa 18 likiwa limejikita zaidi katika kuibua vipaji na kuendeleza utambulisho wa mitindo ya Kiafrika duniani.
Tamasha hilo linalotajwa kuwa miongoni mwa majukwaa makubwa barani Afrika litafanyika Desemba 5–7 jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mwandaaji wa tamasha hilo, Mustafa Hassanal, Swahili Fashion Week limeendelea kuwa kitovu cha mageuzi ya ubunifu barani Afrika—likileta pamoja wabunifu mahiri kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali huku likitoa fursa muhimu kwa vipaji vipya kujitambulisha.
“Kwa miaka yote jukwaa hili limekuwa chachu ya hadithi za Afrika kupitia mitindo. Tumefaulu kuchanganya urithi wa kitamaduni na ubunifu wa kisasa, na hilo limeifanya SFW kuwa taa ya ubunifu katika bara na diaspora,” alisema Hassanal.
Amesema kuwa dira ya SFW ni kuhakikisha ubunifu wa Afrika unafika kwenye viwango vya kimataifa bila kupoteza mizizi ya kitamaduni.
“Mustakabali wa mitindo ni wa Kiafrika, wa kisasa, wa kidijitali na wenye mizizi katika ubunifu,” alisisitiza.
Mbali na maonesho ya mavazi, SFW inaendelea kuwa nguzo muhimu kwa wabunifu chipukizi kupitia shindano la vipaji vipya la Washington Bendella, huku pia ikitoa tuzo 29 kwa wanatasnia na chapa zilizotoa mchango mkubwa katika kukuza sekta ya mitindo.
Msimu huu utawakutanisha wabunifu zaidi ya 50 kutoka Tanzania na nje ya nchi, wakiwemo Mkwandule’son, Tory Eleganza (Dodoma), The Seamy Luxe, Jesakudo, Asili by Naliaka, Bilan Facon, Neith Designs, Zuh Fashion na Pwani Pure.




