Nikitin Dheer: Dharmendra alipiga Simu akiwa ICU

MUMBAI: MUIGIZAJI Nikitin Dheer ameonesha hisia nzito baada ya kifo cha gwiji wa Bollywood, Dharmendra, aliyefariki jana akiwa na umri wa miaka 89.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nikitin alisimulia uhusiano wa karibu uliokuwepo kati ya familia yao na marehemu, akifichua tukio la kipekee ambapo Dharmendra alipiga simu kutoka ICU kutoa pole za kifo cha baba yake, Pankaj Dheer.
Nikitin aliandika kuwa yeye na baba yake walikuwa wakimjadili mara kwa mara Dharmendra kuwa ndiye shujaa katika historia ya filamu za India.
“Baba alipofariki, Dharmendra alipiga simu akiwa chumba cha wagonjwa mahututi ICU kumfariji mama. Alimwambia mama asijali, kwamba angepona na kurejea nyumbani karibuni.”
Nikitin aliongeza kuwa tabasamu la Dharmendra lilikuwa la kipekee, na kila mara alionesha upendo na heshima kwa watu aliokuwa karibu nao.
“Hakuna ataweza kujaza nafasi uliyotuachia. Hakutakuwepo mwingine kama Dharmendra. Pole kwa familia nzima. Pumzika kwa Amani… Aum Shanti.”
Dharmendra, mmoja wa waigizaji maarufu katika historia ya Bollywood, alifariki Novemba 24. Alikuwa ametoka hospitali wiki moja kabla na alikuwa akipata nafuu nyumbani. Alizikwa Mumbai mbele ya familia na watu wa filamu.
Kifo chake kimetajwa kama “mwisho wa enzi”, kutokana na mchango wake mkubwa katika tasnia ya filamu.
Baadhi ya filamu zake mashuhuri ni ‘Sholay, Chupke Chupke’, ‘Satyakam’, ‘Dost’ na ‘Seeta Aur Geeta’. Filamu yake ya mwisho, Ikkis, inatarajiwa kuachiwa Desemba 25, ambapo anaigiza kama baba wa Agastya Nanda.




