Kwingineko

MLS kusimama wiki saba

FLORIDA: LIGI kuu ya Marekani Major League Soccer (MLS) imetenga mapumziko ya wiki saba katika kalenda ya msimu ujao ili kuruhusu wachezaji kushiriki Kombe la Dunia la 2026 litakalofanyika nchini humo na majirani zao Mexico na Canada.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa Alhamisi, ligi hiyo itasimama kuanzia Mei 25 tarehe ya lazima ya kuripoti kwa wachezaji iliyowekwa na FIFA hadi Julai 16 ili kutoa nafasi kwa michuano hiyo ambayo kwa mara ya kwanza itashirikisha timu 48.

Kombe la Dunia litaanza Juni 11, huku fainali pekee itakayochezwa Julai 19 mjini East Rutherford, New Jersey itachezwa baada ya kurejea kwa michezo ya MLS.

Mapumziko haya ya wiki saba ni marefu zaidi kushuhudiwa katika historia ya MLS ikilinganishwa na awali, ambapo kulikuwa na mapumziko ya wiki mbili mwaka 2010 na 2014, na siku tisa mwaka 2018. Msimu wa MLS haukuingiliana na Kombe la Dunia la 2022 lililofanyika Qatar.

Mechi ya ufunguzi itakuwa kati ya Inter Miami na Los Angeles FC kwenye uwanja wa LA Coliseum Februari 21, siku ambayo timu zote 30 zitakuwa uwanjani. Klabu ya Lionel Messi, Inter Miami, itafungua rasmi uwanja wake mpya wenye 25,000 Miami Freedom Park tarehe 4 Aprili katika mchezo dhidi ya Austin FC.

Mchezo wa Nyota wa MLS (All-Star Game) utafanyika Julai 29 mjini Charlotte, North Carolina.

Klabu zote za MLS zitacheza jumla ya mechi 34, 17 nyumbani na 17 ugenini ikiwemo michezo miwili dhidi ya kila mpinzani wa mkondo mmoja na jumla ya sita dhidi ya timu za mkondo tofauti.

Msimu wa kawaida unatarajiwa kumalizika Novemba 7, na playoffs kuanza Novemba 18 baada ya dirisha la kimataifa la FIFA. Hatua za mwisho za msimu zitachezwa bila mapumziko, japokuwa ratiba kamili ya playoffs bado haijatolewa.

Baada ya mwaka 2026, MLS haitaanza tena Februari hadi Desemba. Badala yake, msimu wa mpito wa mechi 14 mwaka 2027 utaandaa njia ya mfumo mpya wa kalenda ya majira ya kiangazi hadi masika (summer-to-spring), unaoendana na ligi nyingi duniani, kuanzia msimu wa 2027–28.

Related Articles

Back to top button