Oscars 2026 kuonesha Tuzo zote 24 ‘Live’

LOS ANGELES: WAANDAAJI wa tuzo za Oscars 2026 wameahidi kutanua wigo wa tuzo hizo na kuongeza ubunifu mbalimbali ikiwemo kuonesha vipengele vyote vya tuzo 24 mubashara.
Waandaaji hao wamethibitisha kwamba kipengele kipya cha ubora katika casting kitaonekana kwenye matangazo ya moja kwa moja ya Tuzo za 98 za Academy Awards mwezi Machi.
Hatua hii inaifanya hafla ya mwaka ujao kuwa na jumla ya tuzo 24, zitakazotolewa moja kwa moja hewani Machi 15. Kati ya hizo ni tuzo maarufu kama Best Picture, Best Actor, na Best Actress, pamoja na zingine zote za kitamaduni.
Pia tuzompya ya ‘Achievement in Casting’ yaingia rasmi katika tuzo hizo.
Bodi ya magavana wa Academy ilitangaza kuanzishwa kwa tuzo ya casting mwaka jana, lakini haikuwa wazi kama ingetangazwa kwenye matangazo ya moja kwa moja tofauti na inavyokuwaga.
Uanzishwaji wa kipengele hiki unakuwa mara ya kwanza Academy kuongeza tuzo mpya tangu Best Animated Feature Film ilipoanzishwa mwaka 2001.
Mwaka huu pia Academy ilitangaza mpango wa kuongeza kipengele kingine Stunt Design Award, kitakachoanza kutolewa kuanzia Oscars za 2028, zitakazoadhimisha Jubilee ya 100.




