Mboso Khan kuja na Pawa Remix

DAR ES SALAAM: Msanii mahiri wa Bongo Fleva, Mbwana Kilungi ‘Mboso Khan’, anatarajia kuachia wimbo wake mpya “Pawa Remix” usiku wa leo saa sita kamili (00:00).
Hii inakuja baada ya toleo la awali la wimbo “Pawa” kufanya vizuri na kushika chati mbalimbali, jambo lililompa msanii huyo sababu ya kuongeza moto kwenye kiwanda cha muziki wa Bongo Fleva.
Taarifa zilizowekwa kupitia ukurasa rasmi wa Khan Music Instagram zimethibitisha kuwa remix hii imepambwa na wakali watatu wenye jina kubwa katika gemu:
Darassa, Billnass na Gnako, ambao wamepewa nafasi ya kuongeza mitazamo na vionjo vyao tofauti kwenye wimbo huo.
Hata kabla ya wimbo kutoka, mashabiki na wadau wa burudani tayari wanaitabiria kufanya vizuri, wakiamini kolabo hiyo itatikisa mitandao ya kijamii kutokana na uzito wa majina yaliyojihusisha.
Kwa sasa mashabiki wameanza kuhesabu saa kuelekea uzinduzi huo, huku mitandao ya kijamii ikianza kujaa tagi kama RN3 PawaRemix Pawa KhanMusic ambazo zimeanza kushika kasi kwenye trending.




