Arsenal yamalizana na Visit Rwanda

KIGALI: BODI ya Maendeleo ya Rwanda (Rwanda Development Board – RDB) imetangaza kuwa itasitisha mkataba wake wa ushirikiano na klabu ya Ligi Kuu ya England, Arsenal, mwishoni mwa msimu huu kwa makubaliano ya pande zote mbili.
Ushirikiano huo, uliojulikana kama “Visit Rwanda,” ulianza miaka nane iliyopita, lakini umezidi kukosolewa kutokana na kuongezeka kwa ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo inapakana na Rwanda.
DRC inaituhumu Rwanda kwa kuwapa silaha na kuwaunga mkono wanamgambo wa M23, ambao wameteka sehemu kubwa ya eneo la mashariki mwa Kongo tangu walipoanza mapigano mwaka 2021.
Mzozo huo umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuzua mgogoro mkubwa wa kibinadamu, ingawa DRC na M23 wametia saini makubaliano ya kusitisha mapigano na mfumo wa amani katika miezi ya hivi karibuni.

Mapema mwezi Aprili, mashabiki wa Arsenal waliandamana kupinga ushirikiano huo, ambao ulijumuisha nembo ya ‘Visit Rwanda’ kuvaliwa kwenye mikono ya jezi za wachezaji.
Katika taarifa yake, RDB imesema: “Arsenal na Bodi ya Maendeleo ya Rwanda zimekubaliana kwa pamoja kumaliza ushirikiano wao mwishoni mwa msimu huu, na hivyo kufunga ushirikiano wa misimu minane ulioifanya ‘Visit Rwanda’ kuwa Mshirika rasmi wa kwanza wa Mikono ya Jezi wa Arsenal.”
Licha ya uamuzi huu, Rwanda bado inaendelea na mikataba mingine ya ushirikiano na klabu kubwa za Ulaya kama vile Paris Saint-Germain, Bayern Munich, na Atletico Madrid




