Featured

Robertson: Natamani Jota angekuwepo Marekani

GLASGOW: Beki wa Liverpool na nahodha wa timu ya taifa ya Scotland Andy Robertson amesema alikuwa huzuni kubwa kabla ya Scotland kuibuka na ushindi wa 4-2 dhidi ya Denmark na kufuzu Kombe la Dunia 2026, akifichua kuwa mawazo yake yalikuwa yakirudi mara kwa mara kwa aliyekuwa mchezaji mwenzake wa Liverpool, Diogo Jota, na ndoto yao ya pamoja ya kucheza katika jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.

Ushindi huo, uliotokana na mabao ya Scott McTominay, Lawrence Shankland, Kieran Tierney na Kenny McLean, uliihakikishia Scotland tiketi ya Kombe la Dunia 2026 litakalofanyika Marekani, Canada na Mexico na kuhitimisha ukame wa miaka 28 bila kushiriki mashindano hayo tangu waliposhiriki mara ya mwisho mwaka 1998.

Jota, aliyefariki katika ajali ya gari mwezi Julai akiwa na miaka 28, hakushiriki Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar kutokana na jeraha. Robertson akisema wawili hao mara nyingi waliwahi kutafakari siku ambayo wangeonekana kwenye Kombe la Dunia pamoja.

“Nimekuwa nikijaribu kuficha, lakini leo nimekuwa kwenye hali ngumu. Namjua vizuri rafiki yangu Jota na leo sikuweza kumtoa kichwani. Umri wangu huu, najua huenda hii ndiyo nafasi yangu ya mwisho kufika Kombe la Dunia.” – Robertson ameiambia BBC.

“Tulizungumza mara nyingi kuhusu kutimiza ndoto hii, baada ya wote kukosa Kombe la Dunia lililopita. Najua leo angejivunia. Ninafurahi kwamba safari hii imefika hapa.”

Robertson pia aliwamwagia sifa wachezaji na benchi la ufundi, akisema umoja wao umeifanya safari hii kuwa ya kipekee.

“Hii ndio timu bora zaidi kuwahi kuwa nayo. Nasaha za kocha kabla ya mchezo zilikuwa za kuhamasisha mno, tuliguswa sana. Huu utabaki kuwa mmoja wa usiku bora zaidi wa maisha yangu.”

Wakati huo huo, Ureno taifa alilotumikia Jota nayo ilifuzu Kombe la Dunia la 2026 Jumapili baada ya kuichapa Armenia 9-1.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button