Czech yailima adhabu Timu ya Taifa

PRAGUE: SHIRIKISHO la soka la Jamhuri ya Czech limeipa adhabu timu ya taifa hilo kwa kumvua unahodha Tomáš Souček na kuwanyima wachezaji wenzake posho zao kama adhabu kwa kupuuza mashabiki wao baada ya mchezo wa mwisho wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Gibraltar.
Wachezaji wa Czech, ambao tayari walikuwa wamejihakikishia nafasi ya pili katika Kundi L, walishinda mchezo wa nyumbani 6-0 mjini Olomouc Jumatatu, lakini hawakwenda kuwashukuru mashabiki waliokuwa wamejitokeza kufuatia ukosoaji wao juu ya kiwango na ubora wa timu katika kampeni hiyo ya kufuzu.

Timu hiyo sasa itakodolea macho droo ya mechi za ‘Playoff’ kesho Alhamisi inayojumuisha timu 16 inayotarajiwa kupigwa Machi mwaka ujao, ambapo nafasi nne za Ulaya katika Kombe la Dunia la 2026 zitawaniwa.
Shirikisho liliwaomba radhi mashabiki na kusema kuwa wachezaji hawatapokea posho za mchezo huo. Badala yake, fedha hizo zitatolewa kwa mashirika ya misaada. Souček atapokonywa unahodha kwa mchezo unaofuata wa timu.
“Mashabiki wana haki kamili ya kuonesha kutoridhishwa kwao na kiwango kisichoridhisha katika mechi za karibuni, Mwitikio wa wachezaji ulipaswa kuwa tofauti kabisa. Walipaswa kuwashukuru mashabiki waliowapa sapoti.” shirikisho limesema kwenye taarifa yake.
Katika mchezo wa Jumatatu, mashabiki walisikika mara kadhaa wakiimba “Pigania Czechia.”.





