Jux kuibuka na ‘Dar to Lagos’ Desemba 18

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Juma Mkambala maarufu kama Jux, anatarajia kufanya tamasha lake kubwa la kimataifa lijulikanalo kama “Dar to Lagos” litakalofanyika Desemba 18, 2025, nchini Nigeria.
Jux, ambaye hivi karibuni alifunga ndoa na mpenzi wake Priscilla Ojo, amesema ana furaha kubwa kwa mapokezi mazuri anayoyapata kutoka kwa mashabiki wa muziki nchini humo, hususan jijini Lagos.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Jux ameshiriki video ya tangazo la tamasha hilo huku akieleza hisia zake kwa mashabiki wa Naija na kuwaahidi onyesho la kipekee.
“Upendo na sapoti ambayo ninyi nyote mmenionyesha umekuwa wa ajabu sana! Najisikia kama niko nyumbani hapa Nigeria.
Kila jiji lina mdundo wake, lakini Lagos lina roho. Tarehe 18 Desemba tunakuja kwa ukubwa tukileta upendo wote, maisha, na urithi pamoja! Kutoka Tanzania hadi Nigeria, moja kwa moja,” ameandika Jux.
Msanii huyo ameongeza kuwa tamasha hilo halitakuwa tukio la muziki pekee, bali ni mkutano wa kifamilia unaounganisha watu kupitia upendo na “positive vibes.”
Jux ameweka video ya matangazo ya tamasha hilo, walionekana pia mke wake Priscilla, mama mkwe wake Iyabo Ojo (ambaye ni muigizaji maarufu wa Nollywood), pamoja na mastaa kadhaa wa Nigeria waliounga mkono tukio hilo.
Ndoa ya Jux na Priscilla imeonekana kumfungulia milango mipya ya mafanikio kwa upande wa kimuziki na kibiashara, na kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni kati ya Tanzania na Nigeria, kupitia kaulimbiu yake ya “Dar to Lagos.”




