Kwingineko

Ederson afichua kilichomuondoa Man City

LONDON: MLINDA lango wa timu ya taifa ya Brazil Ederson Moraes amesema alijaribu kuondoka Manchester City mara kadhaa kabla ya msimu uliopita, akifichua kuwa ni kutokana na kukosa furaha ndani ya kikosi cha Pep Guardiola kulikochangiwa sana na majeraha ya mara kwa mara yaliyomfanya ashindwe kufurahia maisha ndani ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Senegal utakaochezwa Jumamosi, kipa huyo mwenye umri wa miaka 32 alizungumzia uhamisho wake kwenda Fenerbahçe, baada ya kujiunga na klabu hiyo ya Uturuki kwa dau la takribani pauni milioni 12 akihitimisha miaka minane yenye mafanikio makubwa jijini Manchester.

Ederson alitwaa jumla ya mataji 18 akiwa na Manchester City tangu ajiunge akitokea Benfica mwaka 2017 yakiwemo mataji sita ya Ligi Kuu ya England na la moja kombe la Carabao na ligi ya Mabingwa Ulaya. Pia amewahi kushinda tuzo ya Golden Glove mara tatu.

“Msimu uliopita nilikuwa tayari nimejaribu kuondoka, lakini sikufanikiwa. Nadhani hilo liliathiri kiwango changu kiasi fulani. Nilipata majeraha matano na sikuwa katika hali bora.” – Ederson amewaambia waandishi wa Habari baadae Jumatano.

“Kitu hicho kilinifanya nihisi nimechoka. Nilizungumza na familia yangu, na tukakubaliana kwamba kama klabu itakubali, ningetafuta changamoto mpya. Hakuna maana ya kubaki kwenye klabu kubwa yenye mafanikio kama huna furaha,” – aliongeza.

“Ni bora kubadilisha mazingira. Sasa napumua mpira tena, nahisi nguvu na msisimko wa mashabiki nchini Uturuki ambao ni wazimu kweli. Nimefurahia sana changamoto hii mpya na nina hamu ya kushinda tena.”

Brazil tayari imejihakikishia ushiriki wake katika Kombe la Dunia la 2026, baada ya kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Paraguay mwezi Juni.

Related Articles

Back to top button