Mohamed kushiriki shindano la kutunisha misuli

DAR ES SALAAM: MTUNISHA misuli Abdallah Mohamed ‘Mr Physique’ anatarajia kuiwakilisha nchi katika mashindano makubwa ya kutunisha misuli Afrika yatakayofanyika Novemba 15, mwaka huu Lusaka nchini Zambia .
Hatua hii inaendeleza ukuaji wa mchezo huo nchini, sambamba na jitihada za wadau na serikali kuuwezesha.
Ofisa Michezo Mwandamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu amemtakia kila la heri mwanamichezo huyo akisema anaamini amefanya maandalizi mazuri kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
“Maandalizi ambayo umeyafanya ambayo sisi BMT tulikuwa tukiyaratibu umejiandaa vizuri, tuna uhakika utashinda, niwaombe Watanzania walioko Zambia wajitokeze siku hiyo kukuunga mkono,”alisema Maguzu.
Maguzu alihimiza pia, wadau na makampuni mbalimbali wanaotaka kudhamini mchezo huo kujitokeza ili kusaidia katika harakati za kukuza vipaji vya mchezp huo.




