Kizz Daniel aibua vurugu baada ya kuchelewa jukwaani

MSANII nyota wa Afrobeat kutoka Nigeria, Kizz Daniel, ameripotiwa kuchelewa kufika kwenye tamasha lake lililofanyika mjini Paris, Ufaransa, jambo lililosababisha vurugu na malalamiko makubwa kutoka kwa mashabiki na waandaaji wa onesho hilo.
Tamasha hilo lilikuwa limepangwa kuanza saa 1 jioni (7:00 p.m.) na kumalizika saa 5 usiku (11:00 p.m.), huku ukumbi ukitakiwa kufungwa saa 6 kamili usiku (12:00 a.m.). Hata hivyo, mashabiki walishangazwa baada ya Kizz Daniel kuonekana jukwaani saa 5:50 usiku (11:50 p.m.), muda ambao kila kitu kilipaswa kuwa kimekwisha.
Mashabiki walianza kufika mapema kuanzia saa 10 jioni (4:00 p.m.), lakini baada ya kusubiri kwa zaidi ya saa kadhaa bila taarifa yoyote, wengi walikerwa na kuanza kuondoka, huku wengine wakilalamika vikali na kuzusha kelele ndani ya ukumbi.
Kwa mujibu wa waandaaji wa tamasha hilo, Kizz Daniel alilipwa zaidi ya ₦140,000,000 (sawa na takriban Sh milioni 239) kwa ajili ya onesho hilo, lakini kuchelewa kwake kulisababisha vurugu kubwa zilizopelekea polisi kuingilia kati kutuliza hali.
Wakati wa vurugu hizo, iliripotiwa kuwa mmoja wa walinzi wa karibu wa msanii huyo (bodyguard) alishambuliwa, jambo lililoibua taharuki zaidi.
Baada ya tukio hilo, menejimenti ya Kizz Daniel ilitoa ufafanuzi ikieleza kuwa kuchelewa huko kulitokana na changamoto za kiufundi pamoja na ucheleweshaji wa vifaa vya muziki vilivyotakiwa kutumika katika shoo hiyo.
“Tulichelewa kutokana na masuala ya kiufundi ambayo hayakuwa chini ya udhibiti wetu. Tunawaomba radhi mashabiki wote wa Paris kwa usumbufu uliotokea. Kizz Daniel anawapenda na anawaahidi onesho kubwa zaidi hivi karibuni,” ilisema menejimenti kupitia taarifa yao kwa vyombo vya habari.
Tukio hilo limeongeza mjadala kuhusu nidhamu ya wasanii barani Afrika wanapofanya maonesho nje ya nchi, huku mashabiki wakitaka wasanii maarufu kama Kizz Daniel kuzingatia muda na heshima kwa mashabiki wao.




