Ligi Kuu

Geita Gold yaapa ushindi dhidi ya Polisi

GEITA: KOCHA Mkuu wa Geita Gold FC, Zuberi Katwila, amesema kikosi chake kimejipanga kikamilifu kuhakikisha kinapata ushindi kwenye mchezo wa Ligi ya Championship dhidi ya Polisi FC, utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Nyankumbu.

Akizungumza na Spotileo, Katwila alisema mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao, lakini amesisitiza kuwa malengo ya timu ni kupata pointi zote tatu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

“Tunacheza na Polisi, timu ambayo ni nzuri, lakini tumejipanga kupata matokeo. Pointi za kesho ni za msingi ili nasi tuweze kwenda juu,” alisema Katwila.

Kocha huyo aliongeza kuwa lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanarejea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, hivyo kila mchezo ni muhimu kwa safari yao hiyo.

“Malengo yetu ni kuendelea kufanya vizuri na kuwa katika nafasi nzuri ili mwisho wa msimu tuweze kurejea Ligi Kuu,” aliongeza.

Katwila pia alisifu ari na morali ya wachezaji wake, akisema wameonesha “wining mentality” katika mazoezi na mechi za karibuni, jambo linalompa matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa kesho.

“Mechi itakuwa ngumu, lakini vijana wangu wana morali na akili ya ushindi. Naamini watafanya vizuri kesho,” alisema.

Geita Gold, ambayo ilishuka daraja msimu wa mwaka juzi inatazamiwa kutumia mchezo huo kama sehemu ya kuonesha dhamira yao ya kurejea katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2026/27.

Related Articles

Back to top button