TFF yawaponza waamuzi 17, waburuzwa mahakamani

ISTANBUL: Mamlaka nchini Uturuki zimeamuru kukamatwa kwa watu 21, wakiwemo waamuzi 17 na mwenyekiti wa klabu moja ya Ligi Kuu nchini humo (Turkish Super Lig), kufuatia uchunguzi wa madai ya kubet na upangaji wa matokeo ya mechi za soka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotangazwa na shirika la habari la serikali, Anadolu Agency, tayari watu 18 kati ya 21 wamekamatwa katika oparesheni hiyo iliyofanyika kwenye miji 12 nchini humo.
Hatua hiyo inakuja wiki moja tu baada ya Shirikisho la Soka la Uturuki (TFF) kuwasimamisha waamuzi 149 na wasaidizi wao, kufuatia uchunguzi uliobaini kwamba baadhi ya maafisa waliokuwa wakichezesha mechi kwenye ligi za kitaifa walihusishwa na michezo ya kubashiri.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Istanbul ilisema waamuzi hao 17 wanachunguzwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na kupanga matokeo, huku rais wa klabu moja ya Super Lig, mmiliki wa zamani wa klabu, na rais wa zamani wa chama cha soka wakiamriwa pia kukamatwa kwa tuhuma zinazofanana.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa mtu mwingine anatafutwa kwa kosa la kusambaza taarifa za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii.
Wakati huo huo, katika uchunguzi wa ndani, kamati ya nidhamu ya TFF imewapa maafisa 149 adhabu za kufungiwa kati ya miezi nane hadi 12 kutokana na ushiriki wao katika shughuli za kubet.

Rais wa TFF, Ibrahim Haciosmanoglu, aliielezea hali hiyo kama “mgogoro wa maadili katika soka la Uturuki.”
Uchunguzi huo umebaini kuwa kati ya waamuzi 571 wanaohusika katika ligi, 371 walikuwa na akaunti za kubet, huku 152 kati yao wakibainika wakibet kwa ufanisi na kushinda mamilioni ya fedha.
Taarifa pia zinaonesha kwamba mmoja wa waamuzi alibet mechi 18,227, huku waamuzi 42 wakibet zaidi ya mechi 1,000 kila mmoja na wengine wachache wakibet mara moja pekee.




