EPL

Dyche aingia jikoni kuipika Forest

NOTTINGHAM: KOCHA mkuu mpya wa Nottingham Forest Sean Dyche amesema kuchukua mikoba ya ukocha wa klabu hiyo ‘kunakamilisha duara’ la safari yake ya soka, baada ya hapo awali kuwa mchezaji chipukizi katika klabu hiyo chini ya kocha mashuhuri wa kihistoria, Brian Clough.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 amekuwa meneja wa tatu wa Nottingham Forest msimu huu, akichukua nafasi ya Ange Postecoglou, aliyeondolewa baada ya siku 39 tu tangu kumrithi Nuno Espirito Santo.

Aliyewahi kuwa kocha wa Watford, Burnley, na Everton, Dyche anakabiliwa na jukumu la kuinusuru Nottingham Forest na mwenendo mbaya wa matokeo katika Ligi Kuu ya England, ingawa kazi yake itaanzia kwenye mchezo wa Europa League nyumbani dhidi ya Porto baadaye leo Alhamisi.

Akizungumza na wanahabari kwa mara ya kwanza Jumatano, Dyche amesema anajivunia kuinoa klabu hiyo yenye mataji mawili ya Ulaya, ambako alianza taaluma yake kama mchezaji wa vijana mwishoni mwa miaka ya 1980.


“Nina historia ndefu na klabu hii, nilikuwepo hapa kati ya mwaka 1987 hadi 1990. Nakumbuka kutembea kando ya Mto Trent huku mbwa wa Clough, Del Boy, akikimbia na sauti ya Brian Clough ikiwa karibu”.

“Wakati huo kulikuwa na wachezaji wakubwa, majina ya hadhi ya juu, na nilikuwa nikijiwazia siku moja kuvaa jezi ya timu hii. Sasa, miaka mingi baadaye, kuwa hapa kama meneja ni jambo kubwa sana kwangu. Lakini sipo hapa kwa ajili ya burudani kuna kazi ya kufanya.” – Dyche aliwaambia waandishi wa habari

Kocha huyo ambaye aliondoka Everton Januari mwaka huu baada ya miaka miwili ya kukinoa kikosi hicho, atasaidiwa na wachezaji wa zamani wa Nottingham Forest akiwemo Ian Woan, Steve Stone, Tony Loughlan, na Billy Mercer.

“Wao wana historia kubwa zaidi hapa kuliko mimi, lakini kwa sasa mambo yamebadilika sana hii ni klabu tofauti kabisa,” aliongeza Dyche.

Chini ya Nuno Espirito Santo, Forest ilimaliza nafasi ya saba msimu uliopita wa Ligi Kuu, ikiwa imewahi hata kuwania nafasi za Ligi ya Mabingwa.

Hata hivyo, mtindo wa kucheza wa Postecoglou uliojaa mashambulizi uliambulia patupu, na sasa Dyche anayejulikana kwa mbinu zake za moja kwa moja (direct football) ameulizwa ni nini mashabiki wa Forest wanaweza kutarajia kutoka kwake.

“Tunapaswa kurejea kwenye njia ya ushindi,” alijibu Dyche, ambaye uzoefu wake pekee wa ukocha kwenye mashindano ya Ulaya ni hatua ya mtoano ya Europa League mwaka 2018 akiwa na Burnley.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button