Kwingineko

Zimbabwe yampa Mjerumani mkono wa kwaheri

HARARE: SHIRIKISHO la Soka la Zimbabwe (ZIFA) limemfuta kazi kocha wake raia wa Ujerumani, Michael Nees, kufuatia kampeni duni ya kufuzu Kombe la Dunia huku ikiwa imesalia miezi miwili pekee kabla ya timu hiyo kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Morocco.

Nees alikuwa ameiongoza timu hiyo kwa miezi 14, kipindi ambacho alihakikisha Zimbabwe inafuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika nchini Morocco. Baada ya hapo, alisimamia mechi sita za mwisho za hatua ya kufuzu Kombe la Dunia la 2026, ambako Zimbabwe ilimaliza mkiani mwa kundi lake, baada ya kutoka sare mechi tatu na kupoteza tatu.

Kwa jumla, Nees alishinda mechi mbili pekee kati ya 14 alizoiongoza timu hiyo ya taifa la kusini mwa jangwa la Sahara tangu alipoteuliwa Agosti mwaka jana.

Zimbabwe sasa inalazimika kumsaka kocha mpya kwa wakati, ili kuiongoza timu hiyo kwenye michuano ya AFCON, ambako watakutana na Misri katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi B utakaochezwa mjini Agadir Desemba 22.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 58 hapo awali aliwahi kufundisha timu za taifa za Seychelles na Rwanda, na pia alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi katika nchi za Israel na Kosovo.

Related Articles

Back to top button