Bundesliga

“Kane amejibadilisha Mwenyewe” – Kompany:

MUNICH: KOCHA wa mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich, Vincent Kompany, amesema mafanikio ya straika wake Harry Kane msimu huu hayahusiani na mbinu au maelekezo yake, bali ni matokeo ya bidii na njaa ya mafanikio aliyojijengea mwenyewe.

Kane ameanza msimu kwa kiwango cha juu, akifunga mabao 11 katika michezo sita ya Bundesliga na kufikisha mabao 18 katika mashindano yote, huku Bayern ikibaki na rekodi ya ushindi katika mechi zake zote 10 za msimu huu.

Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya England pia ameifungia nchi yake mabao mawili katika ushindi wao wa 5–0 dhidi ya Latvia, uliowahakikishia nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia la 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Der Klassiker dhidi ya Borussia Dortmund utakaopigwa kesho Jumamosi, Kompany amesema mafanikio ya Kane ni matokeo ya nidhamu binafsi.

“Harry amejifikisha kwenye kiwango hicho mwenyewe. Hiyo ni matokeo ya juhudi na mtazamo wa ushindi. Ameshughulika kila mwaka kujiboresha. Huenda kukosa mataji katika miaka ya awali kulimfanya abaki na njaa ya mafanikio unayoiona leo.” – amesema Kompany

Kane, mwenye umri wa miaka 32, alikuwa hajashinda taji lolote akiwa na klabu yake ya zamani ya Tottenham Hotspur, kabla ya kuvunja nuksi hiyo msimu uliopita kwa kutwaa taji la Bundesliga akiwa na Bayern.

Kompany sasa anatumai nahodha huyo wa England ataendeleza makali yake kwenye mchezo wa wikendi hii dhidi ya Dortmund, ambao wapo alama nne nyuma ya vinara hao na hawajapoteza mechi yoyote katika mashindano ya ndani na Ulaya msimu huu.

Related Articles

Back to top button