Rodrygo, Vini jr kimeeleweka Brazil

MADRID: Washambuliaji wa Real Madrid, Rodrygo na Vinícius Jr, wameitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kitakachocheza mechi za kirafiki dhidi ya Korea Kusini na Japan mwezi huu, huku Neymar akikosa kutokana na jeraha la paja.
Vinícius aliachwa nje ya kikosi cha Carlo Ancelotti kilichocheza mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Chile na Bolivia mwezi uliopita, wakati Rodrygo mara ya mwisho kuichezea Brazil ilikuwa mwezi Machi. Eder Militão pia amerejea kikosini baada ya kupona jeraha la muda mrefu la goti.
Neymar, anayeshikilia rekodi ya mfungaji bora wa Brazil, alipata jeraha la misuli ya paja mwezi uliopita na anatarajiwa kurejea uwanjani mwezi Novemba.
Kipa Alisson, beki Marquinhos na mshambuliaji Raphinha wote pia hawajajumuishwa katika kikosi hicho kwa sababu ya majeraha.
Brazil watakabiliana na Korea Kusini jijini Seoul Oktoba 10, kabla ya kusafiri kwenda Tokyo kukutana na Japan siku nne baadaye.
Ancelotti amesema kikosi kilichoitwa siyo orodha ya mwisho ya wachezaji watakaosafiri Kwenda Marekani kwa ajili ya Kombe la Dunia mwakani hivyo wachezaji wanapaswa kujituma na kujihakikishia nafasi.
“Ni wazi, wengi wa hawa wachezaji watakuwepo Kombe la Dunia, lakini hii ni orodha ambayo pia imezingatia majeraha tuliyopata siku za karibuni, Ni nafasi kwa wengine kuonyesha ubora wao.” – alisema.