
DAR ES SALAAM:MSANII wa Bongo Fleva William Lyimo maarufu kama Billnass amekanusha tetesi zilizoenea mitandaoni kuhusu kuvunjika kwa ndoa yake na mkewe, Faustina Mfinanga ‘Nandy’.
Akizungumza na Spoti Leo Billnass amesema kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na kwamba watu wanaosubiri kuona wakiachana watalazimika kusubiri sana.
“Hatujaachana, mambo ya mitandaoni ni ya mitandaoni jamani. Wanaotaka sijui yametokea wapi kuhusu kuachana, na wanaotaka tuachane watasubiri sana,” amesema Billnass
Tetesi hizo ziliibuka baada ya mashabiki kugundua kuwa wawili hao walifuatana na kuacha kufuatana kwenye mitandao ya kijamii, jambo lililoibua tafsiri kwamba huenda ndoa yao iko mashakani.
Hata hivyo, Billnass alibainisha kuwa kufuatana au kuacha kufuatana Instagram si hoja ya msingi katika maisha yao ya ndoa, akisisitiza kuwa familia yao ipo imara.
Kwa upande wake, Nandy hakupokea simu inaita tu uwenda angepokea tungepata ufafanuzi wa kina kuhusu madai hayo.
Pamoja na uvumi huo, miezi michache iliyopita wawili hao walisherehekea kumbukumbu ya miaka mitatu ya ndoa yao, ambapo Billnass alimkabidhi Nandy pete mpya baada ya ile ya awali kupotea, ishara kuwa bado wanadumisha upendo wao.