APR FC, Singida BS na KMC wagusa nusu fainali Kagame

DAR ES SALAAM: TIMU tatu zimefanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali katika mashindano ya CECAFA Kagame Cup 2025 yanayoendelea Dar es Salaam.
Timu hizi ni APR FC ya Rwanda, na klabu mbili za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Singida Black Stars FC na KMC FC.
APR FC, washindi wa fainali mwaka 2024, walimaliza kwa sare ya 1-1 dhidi ya KMC FC katika mchezo wa Kundi B uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Jana.
Timu zote mbili zilikusanya pointi 7, lakini APR FC walimaliza kileleni huku KMC FC wakiwa timu bora ya nafasi ya pili baada ya kuzingatia pointi za makundi mengine.
Katika mchezo mwingine wa Kundi B uliofanyika kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo Zanzibar, mabingwa wa Zanzibar, Mlandege FC, waliibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Bumamuru FC ya Burundi.
Singida Black Stars FC, ambao pia wanawakilisha Tanzania kwenye CAF Confederation Cup 2025/2026, walifikia nusu fainali baada ya kumaliza kileleni Kundi A wakiwa na pointi 7.
Timu ya kocha Miguel Gamondi ilishinda 1-0 dhidi ya Garde Cotes ya Djibouti katika mchezo wao wa mwisho kwenye Uwanja wa KMC.
Mchezo mwingine wa Kundi A, Kenya Police Bullets FC waliibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Ethiopian Coffee SC.
Hadi sasa, bado kuna michezo miwili ya Kundi C itakayochezwa Leo Jumatano ili kuamua timu ya mwisho kufuzu nusu fainali. Mogadishu City Club watacheza na Alahly Wad Madani, huku Al Hilal Omdurman wakikabiliana na Kator FC ya Sudan Kusini.
Katika nusu fainali, APR FC watawakabili washindi wa Kundi C, huku Singida Black Stars wakikabiliana na KMC FC.
Mashindano ya CECAFA Kagame Cup 2025 yamefadhiliwa na Betika, huku Rais wa Rwanda, Paul Kagame, akitoa dola za Marekani 60,000 kwa jumla ya zawadi za fedha sawa na zaidi ya sh milioni 100.




