“Vita baridi na Isak haitusaidii” – Howe

BIRMINGHAM: MENEJA wa Newcastle United Eddie Howe amekiri kuwa vita baridi iliyopo baina ya klabu hiyo na mshambuliaji anayetaka kuondoka Alexander Isak haina faida yeyote kwa klabu hiyo wakati huu timu yake ikijiandaa kuanza msimu wa Ligi Kuu bila mfungaji huyo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden mwenye umri wa miaka 25, ambaye amefunga mabao 62 katika michuano yote tangu alipowasili kwa ada iliyoweka rekodi ya klabu mwaka 2022, anaonekana kutoyumba na dhamira yake ya kuondoka Newcastle katika dirisha hili la usajili.
Tetesi zinasema kuwa bingwa mtetezi Liverpool alikuwa tayari kutoa ofa ya pauni milioni 110 ambayo ni sawa na shilingi za Kitanzania Bilioni 346.5 iliyokataliwa na Newcastle kwa Isak, ambaye alifunga mabao 23 msimu uliopita na kuisaidia Newcastle kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Haijawa sawa, sidhani kama imekuwa afya kikosini sitabisha kumekuwa na changamoto kubwa mno. Alex ni mmoja wa washambuliaji bora zaidi duniani, kwa hiyo kumkosa kwenye kikosi ni pengo kubwa. Bado hatuna uhakika lakini itabidi tutafute namna ya kushinda bila yeye Villa Park.” – Howe aliiambia BBC.
Howe amekiri kwamba morali ya kikosi iliongezeka wakati wa maandalizi ya msimu mpya (Pre-season) Isak alipofanya mazoezi peke yake katika klabu yake ya zamani ya Real Sociedad, Newcastle walipokuwa ziarani barani Asia.
Amesema lazima kuwe na ugumu mwanzoni mchezaji muhimu kama huyo anapoondoka lakini wachezaji wanazoea na morali ya kikosi inapanda kila siku. Tayari kuna taarifa za Mshambuliaji huyo kutokuwa sehemu ya kikosi kitakachoivaa Aston Villa kesho Jumamosi.