Pazia la Ligi Kubwa Barani Ulaya kufunguliwa Leo

Pazia la ligi mbalimbali barani Ulaya linafunguliwa leo kwa michezo ya ufunguzi yenye msisimko mkubwa kwa mashabiki wa soka kote ulimwenguni. Ligi Kuu ya England (EPL), Ligi Kuu ya Hispania (LaLiga), pamoja na Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), zote zikishuhudia michezo yake ya ufunguzi leo usiku.
Katika Ligi Kuu ya England, mabingwa watetezi wa taji hilo Liverpool watafanya uzinduzi wa msimu mpya katika dimba la Anfield dhidi ya AFC Bournemouth, ambao walimaliza nafasi ya 9 msimu uliopita. Mchezo huu unabeba hisia nyingi za mashabiki wa Liverpool, ukitarajiwa kujumuisha dakika ya maombolezo kwa mshambuliaji wao, Diogo Jota, aliyefariki mwezi Juni.
Liverpool imeshinda michezo minne kati ya mitano iliyopita baina ya timu hizi, ambapo ushindi wa hivi karibuni zaidi uliwahi kuchezwa tarehe 1 Februari mwaka huu, Mohamed Salah akifunga mabao yote mawili ya mchezo huo. Mchezo huu pia utawapa fursa wachezaji wapya kama Florian Wirtz, Hugo Ekitiké, Jeremie Frimpong, na Milos Kerkez kuonekana mbele ya mashabiki, huku Ryan Gravenberch akikosekana kutokana na kadi nyekundu ya msimu uliopita.

Ligi Kuu ya Hispania (LaLiga) itaanza kwa kishindo cha mechi mbili. Mapema, CF Girona watakuwa nyumbani katika dimba la Estadi Municipal de Montilivi, kuwakabili Rayo Vallecano kuanzia saa mbili usiku. Baada ya hapo, Real Oviedo waliopanda daraja watakuwa wageni wa Villarreal katika dimba la Estadio de la Cerámica kuanzia saa nne usiku.
Kwa upande wa Ligue 1 ya Ufaransa, wababe Marseille watakuwa wageni wa Stade Rennes katika dimba la Roazhon Park katika mchezo wa ufunguzi wa msimu mpya. Katika michezo mitano iliyopita baina ya timu hizi, Marseille imefanikiwa kushinda mitatu, Rennes mmoja, na kumaliza sare moja.




