
KOCHA Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Pluijm amewataka wachezaji wa klabu yake kudhihirisha ubora wao kwa kuifunga Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Novemba 9 uwanja wa LITI mkoani Singida.
Akizungumza na SpotiLeo kwa njia ya mtandao wa kijamii wa Facebook leo, kocha huyo raia wa Uholanzi amesema timu yake inataka ubingwa na raha ya kubeba ubingwa lazima kuzifunga timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam sababu ndizo zenye malengo ya ubingwa.
“Ni mchezo mgumu sababu tunacheza na timu yenye uzoefu wa ligi lakini Singida pia ni timu kubwa yenye uwezo wa kucheza na timu yoyote Tanzania ikiwemo Simba. Wachezaji wetu wanatakiwa kuthibitisha hilo ili kuongeza heshima yao na timu,” amesema Pluijm.
Kocha huyo amesema wachezaji wake akiwemo mshambuliaji Meddie Kagere wameahidi kuleta furaha baada ya dakika 90 za mchezo huo.
Timu hizo zitakutana huku zikiwa zinalingana kwa pointi lakini Singida ipo nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 17 sawa na Simba iliyopo nafasi ya pili zikitofautishwa na uwiano wa mabao.

Mchezo mwingine wa Ligi Kuu Novemba 9 ni kati ya Azam na Dodoma Jiji katika uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Azam ipo nafasi ya 3 ikiwa na pointi 17 baada ya michezo 9 wakati Dodoma Jiji inashika nafasi 14 ikiwa na pointi 6 baada ya michezo 9.
				
					



