Mbundwike, Ezra waing’arisha Tanzania Comoros

COMOROS: MABONDIA wa Timu ya Taifa ya Ngumi ya Tanzania “Faru Weusi” wameweka historia mpya katika mashindano ya Kombe la Rais yaliyofanyika visiwa vya Comoros, baada ya kutwaa medali za Dhahabu kupitia Kassim Mbundwike (75kg) na Ezra Paulo (60kg), na kuiwezesha Tanzania kumaliza nafasi ya pili kwa ujumla.
Mapambano hayo ya fainali yaliyomalizika juzi kwenye Uwanja wa Malouzini, yamehudhuriwa na Rais wa Comoros Azali Assoumani, ambapo Mbundwike alimtwanga mpinzani wake Soilihi Anzali kwa pointi 2-1, huku Ezra Paulo naye akishinda kwa alama hizo hizo dhidi ya Radjay Mohamed.
Kwa ushindi wao, mabondia hao walipewa zawadi ya simu janja kutoka kwa mdhamini mkuu Kampuni ya YAS, pamoja na vikombe vya uchezaji bora wa mashindano.
Katika mapambano mengine, mabondia Kaimu Kaimu (54kg) na Rashid Mrema (63.5kg) walipata medali za fedha baada ya kupoteza kwa pointi 2-1 dhidi ya wapinzani wao kutoka Comoros – Mohamed Ali na Ilzam Taoufik.
Tanzania ilinyakua kombe la mshindi wa pili kwa ujumla, nyuma ya wenyeji Comoros waliomaliza wa kwanza. Nchi nyingine shiriki zilikuwa Gabon na Madagascar zilizoshika nafasi ya tatu na nne mtawalia.
Katika upande wa uamuzi na marefa, Mwamuzi na Jaji wa Kimataifa wa Nyota Moja, Ramadhani Mazola, alitangazwa kuwa mwamuzi bora wa mashindano miongoni mwa waamuzi 12 waliokuwa wakisimamia pambano. Mazola alitunukiwa kikombe, medali na cheti cha kutambua mchango wake mkubwa katika mashindano hayo.
Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Lukelo Willilo, alisema ushindi huo ni matokeo ya jitihada na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika kukuza vipaji na kuwaendeleza wataalamu wa mchezo huo kwa viwango vya kitaifa na kimataifa.
Wakati huo huo, Balozi wa Tanzania nchini Comoros Said Yakubu, aliipongeza timu nzima kwa kuonesha uzalendo na kujituma na kuiletea heshima Tanzania katika mashindano hayo ya kimataifa.




