Ligi Daraja La Kwanza

Makata kurudi kwa kishindo Polisi Tanzania

DODOMA: Timu ya Polisi Tanzania imejipanga kufanya makubwa katika msimu ujao wa Ligi Daraja la Kwanza (Championship) baada ya kumsainisha aliyekuwa kocha wao wa mafanikio Mbwana Makata.

Akizungumza jijini Dodoma, Ofisa Habari wa timu hiyo, Inspekta Frank Lukwaro, alisema hatua ya kumpatia kandarasi mpya Makata imetokana na uzoefu wake mkubwa katika soka la ndani, hasa katika ligi ya Championship.

“Moja ya sababu zilizomfanya apatiwe timu ni uzoefu wake. Hata msimu wa 2018/2019 tulipopanda Ligi Kuu, tulikuwa naye. Hivyo si mgeni kwetu, anatufahamu na sisi tunamfahamu. Tunaamini atakuwa na wakati mzuri,” alisema Inspekta Lukwaro.

Lukwaro alibainisha kuwa tayari Makata amekabidhiwa ripoti ya kikosi cha msimu uliopita ili kumrahisishia kazi ya kuunda kikosi imara. Aliongeza kuwa uongozi umedhamiria kumpa ushirikiano mkubwa kufanikisha lengo la kurejea Ligi Kuu.

“Tunaamini ushirikiano na uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro na wadau wengine utakuwa chachu ya mafanikio. Polisi Tanzania ni timu ya Watanzania wote, tunalenga kuleta ushindani, kukuza vipaji na kuendeleza falsafa ya Polisi Jamii,” alisisitiza Lukwaro.

Makata ambaye amechukua nafasi ya Moussa Rashid, atatambulishwa rasmi hivi karibuni na Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Kamishna wa Polisi Jamii CP Faustine Shilogile, ambapo alisaini mkataba wa miaka miwili kuiongoza timu hiyo.

Related Articles

Back to top button