Arsenal ‘yamnawa’ Tomiyasu

LONDON: Washika mitutu wa jiji la London Arsenal wametangaza kuwa beki wake raia wa Japan Takehiro Tomiyasu ataondoka Arsenal kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya kucheza dakika sita pekee msimu uliopita kutokana na jeraha la goti.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alipata majeraha mengi ya goti na kigimbi cha mguu wakati wa miaka minne katika klabu hiyo ya Kaskazini mwa London, ambayo baadhi yake yalimweka nje kwa miezi kadhaa huku akiendelea kukalia mbao za hospitali tangu alipofanyiwa upasuaji wa goti mapema mwezi Februari.
“Kwa bahati mbaya, majeraha yamepunguza muda wa Tomi uwanjani katika misimu miwili iliyopita, beki huyo amecheza mchezo mmoja tu akitokea kama mchezaji wa akiba msimu uliopita, Kwa hivyo ilikubaliwa baina yetu wote wawili kusitisha mkataba wa Tomi ili aanze sura mpya katika taaluma yake ya soka” Taarifa ya Arsenal imesema.
Mchezaji huyo wa zamani wa Bologna amecheza mechi 65 za Ligi kuu ya England (Premier League) akiwa na Arsenal, akifunga mabao mawili pekee.
Arsenal, ambayo imemaliza katika nafasi ya pili kwenye ligi kwa misimu mitatu iliyopita, wataanza kampeni yao ya msimu 2025/26 dhidi ya mashetani wekundu Manchester United Agosti 17.




