Ligi Kuu

Yanga: Kipaumbele ni ubingwa, sio tuzo binafsi

DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga imeweka wazi kuwa lengo lao kuu kwa sasa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku wakisisitiza kuwa tuzo binafsi za wachezaji si kipaumbele katika hatua ya sasa ya msimu.

Kauli hiyo ya Yanga imekuja huku wapinzani wao wa jadi, Simba, wakijivunia mafanikio ya mchezaji wao Jean Charles Ahoua, anayeongoza mbio za kiatu cha dhahabu akiwa na mabao 16.

Anafuatiwa kwa karibu na washambuliaji wa Yanga, Prince Dube na Clement Mzize, ambao wote wamefunga mabao 13 kila mmoja.

Kwa upande wa makipa, Moussa Camara wa Simba anaongoza kwa kuwa na ‘clean sheets’ 18, akifuatiwa na Djigui Diarra wa Yanga mwenye 16, huku Patrick Munthari wa Mashujaa FC akiwa na 12.

Akizungumza kuhusu mwenendo wa mbio hizo binafsi, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema msimamo wa klabu hiyo ni kwamba wanapambana kwa ajili ya ubingwa, si kwa minajili ya kutengeneza mazingira ya wachezaji binafsi kutwaa tuzo.

“Kipaumbele chetu ni ubingwa wa ligi. Hatuingii uwanjani kwa ajili ya kumtengenezea mabao Dube, Mzize au Pacome.

Tunataka pointi tatu kila mechi. Akifunga Bacca au hata kipa wetu Diarra, Wanayanga watashangilia kwa sababu wanajua bao hilo lina maana ya ushindi,” amesema Kamwe.

Ameongeza kuwa mafanikio ya wachezaji binafsi kama kuwa mfungaji bora, kipa bora au beki bora, yatakuja tu endapo timu itafikia malengo yake makuu ambayo ni kutwaa ubingwa.

Kamwe amesema nguvu kubwa ya klabu kwa sasa imeelekezwa katika kuhakikisha wanashinda mechi zao zilizobaki ili kumaliza msimu wakiwa juu ya msimamo wa ligi.

Yanga imebakiza michezo miwili tu kabla ya msimu kufungwa. Watacheza dhidi ya Dodoma Jiji FC Juni 22 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kabla ya kuvaana na Simba SC katika Kariakoo Derby itakayofanyika Juni 25 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button