Hatuchezi sasa kuhamia Simba

DAR-ES-SALAAM, MECHI ya watani wa jadi maarufu kama Kariakoo Derby imeendelea kuwa kitendawili kigumu wakati huu ambao matamko na taarifa zimekuwa zikipishana kila kukicha huku kukiwa na sintofahamu ya kipute hicho kikubwa zaidi kwenye soka la Tanzania kutapigwa Jumapili ya Juni 15 kama ilivyopangwa kwenye ratiba na bodi ya ligi kuu TPLB
Moto unazidi kukolea baada ya Klabu ya Simba ambao ni wageni wa mchezo huo unaotarajiwa kupigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa kutoa taarifa jioni hii ya kutokubali kuahirishwa tena kwa mchezo huo namba 184 ikiwa itafanyika hawatakuwa tayari kucheza.
Katika taarifa iliyotolewa na klabu hiyo jioni ya leo Juni 12, Simba imeuarifu umma, wanachama na wapenzi wake kuwa itaingia uwanjani siku ya Jumapili, tarehe 15 Juni 2025, kushiriki mchezo namba 184 kama ilivyopangwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa “Mabadiliko yoyote ya kujaribu kuahirisha mchezo huo ni batili na kinyume na taratibu za uendeshaji wa mpira wa miguu”.
“Kwa msingi huo, Klabu ya Simba haitashiriki mchezo wowote wa namba 184 isipokuwa ule uliopangwa kuchezwa siku ya Jumapili, tarehe 15 Juni 2025.”
Simba imekamilisha taarifa hiyo kwa kuwaomba wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kuijaza Benjamin Mkapa siku hiyo muhimu ili kuiunga mkono klabu hiyo.