Sane atimkia Uturuki

ISTANBUL, Winga wa Bayern Munich, Leroy Sane yuko mbioni kukamilisha dili lake la kuhamia katika klabu ya Galatasaray ya Uturuki kama mchezaji huru baada ya mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich kuonekana kutokuwa na nia ya kuendelea nae mkataba wake utakapomalizika baadae mwaka huu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 tayari amewasili katika jiji la Istanbul mapema leo Alhamisi kwa ajili ya vipimo vya afya kabla ya kutia saini mkataba na mabingwa hao wa Super Lig ya nchini humo.
Klabu hiyo ya Uturuki ‘ilipost’ picha kwenye mitandao yake ya kijamii, picha zilizomuonesha Sane akiwa amevaa skafu ya Galatasaray alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Ataturk, ikisema “wameanza mazungumzo ya uhamisho” na Mjerumani huyo.
Zaidi ya wafuasi milioni moja walifuatilia matangazo ya moja kwa moja kwenye chaneli ya YouTube ya Galatasaray siku ya Jumanne ya teknolojia ya ufuatiliaji wa ndege akionesha ndege ya Sane ikianza safari na hadi kuwasili jijini Istanbul.
Sane, ambaye alijiunga na Bayern Munich kwa mkataba wa miaka mitano kutoka Manchester City mwaka 2020, mkataba wake unamalizika Allianz Arena mwishoni mwa mwezi huu na ikiwa atakamilisha usajili huo itakuwa ishara ya wazi ya kushindwa kwa mazungumzo ya kusalia Allianz Arena yaliyokuwa yakiendelea kwa muda mrefu.