Lewandowski ‘amfukuza’ kocha Poland

WARSAW, Kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka ya Poland Michał Probierz ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi yake ya kocha mkuu wa taifa hilo siku chache baada ya kuzozana na mshambuliaji nyota na aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho Robert Lewandowski.
“Baada ya tafakari ya muda na ya kina na kwa kuzingatia hali ya sasa ya timu, na kwa manufaa ya timu ya taifa nimeamua kujiuzulu nafasi yangu kama kocha mkuu wa kikosi hiki,” Michał Probierz alinukuliwa katika taarifa iliyochapishwa na Chama cha Soka cha Poland.
Probierz alimvua kitambaa cha unahodha mshambuliaji huyo wa Barcelona katika usiku wa kuamkia siku ya mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Finland mapema tarehe 8 Juni na kumteua kiungo wa Inter Milan Piotr Zieliński kama nahodha mpya.
Lewandowski alijibu hatua hiyo ya kocha kwa kusema hataichezea tena timu ya taifa kama kocha Probierz ataendelea kuwa kocha mkuu wat imu hiyo. Katika mechi hiyu Poland ilikumbana na kichapo cha aibu cha mabao 2-1 kutoka Finland, na kuweka matumaini yao ya kufuzu hatarini.
Lewandowski mwenye umri wa miaka 36, ameichezea nchi yake rekodi ya michezo 158 na ndiye mfungaji bora wa muda wote akiwa na mabao 85, bila shaka ndiye mchezaji bora zaidi katika historia ya soka ya Poland.
Lewandowski alijiondoa pia kushiriki kwenye mchezo wa kirafiki wa Ijumaa iliyopita dhidi ya Moldova, akisema sababu ya kutocheza ni uchovu wa msimu wa kutwaa ubingwa wa La Liga akiwa na Barcelona.




