Muziki

Miaka 25 ya Lady Jay Dee

Safari ya Ushindi, Mapambano na Kuandika Historia ya Bongo Fleva

DAR ES SALAAM:WASANII wa Bongo Fleva, hasa wanawake, wana mengi ya kujifunza kutoka kwa mwanamuziki mkongwe na mwasisi wa muziki huo kwa upande wa wanawake, Lady Jay Dee, anayetimiza miaka 25 kwenye tasnia ya muziki mwaka huu.

Maadhimisho haya makubwa yatafanyika Juni 13, 2025 katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki.

Lady Jay Dee, anayefahamika pia kwa jina la Jide, ametangaza pia kuachia kitabu kipya kinachoelezea safari yake ya maisha na muziki, kikiwa na simulizi zitakazogusa hisia za wengi kuhusu changamoto, mafanikio, na maisha yake ya kisanii yaliyodumu kwa robo karne.

“Kila siku ninapoongeza miaka sihisi tofauti, najiona yule yule. Changamoto zimekuwa nyingi, lakini leo nimesimama kama nyumba ya dhoruba. Nimezoea,” alisema Jay Dee kwa msisitizo.

Kauli hiyo inaonyesha uthabiti wake sio tu katika uundaji wa muziki wa kipekee, bali pia katika kupambana na vikwazo vya maisha binafsi na tasnia yenyewe.

Jay Dee ameendelea kuwa nguzo thabiti ya Bongo Fleva, akibaki mwaminifu kwa sauti na mtindo wake wa kipekee, huku akitoa nafasi kwa wasanii wengine kujifunza kupitia safari yake.

Miaka 25 ya Lady Jay Dee si hadithi ya kawaida—ni somo la uvumilivu, mapenzi kwa sanaa, na kupigania nafasi ya mwanamke ndani ya muziki. Kwa mantiki hiyo, mashabiki, wanamuziki na wadau mbalimbali wa tasnia ya burudani wanahimizwa kusherehekea sio tu mafanikio yake ya kibinafsi, bali pia mchango wake mkubwa katika kuleta heshima na nafasi ya wanawake kwenye muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania.

Related Articles

Back to top button