Kwingineko

Kane: Kwa timu hii, Bado tuna kazi ya kufanya

NOTTINGHAM: NAHODHA wa timu ya Taifa ya England Harry Kane amesema ikiwa timu hiyo ya taifa inataka kuwepo kwenye mtifuano wa kombe la Dunia lijalo la 2026 ni lazima iboreshe haraka namna inavyocheza ili kuendana na ukubwa wa jina lake ki-soka Duniani

Kane ametoa kauli hiyo baada ya England kulazwa bao 3-1 katika mechi ya kirafiki na Senegal usiku wa kuamkia leo katika dimba la City Ground jijini Nottingham kikiwa ni kipigo cha kwanza kabisa dhidi ya timu ya taifa kutoka bara la Afrika kipigo kilichoibua mashaka kwa kocha wao Thomas Tuchel ikiwa ni mechi nne tu tangu aanze kuiongoza timu hiyo.

“Haitoshi. Tulikuwa na nyakati nzuri katika mchezo huu, lakini tukiwa au bila mpira mambo hayakuwa mazuri, bado hatupati tempo sahihi. Tumepoteza nguvu yetu tuliyokuwa nayo zamani.” – alisema

Kane anaamini kikosi chake kinapitia kipindi cha mpito tangu kuondoka kwa kocha Gareth Southgate baada ya Euro 2024, lakini amesema kuna muda mchache wa kurekebisha mambo kuelekea Kombe la Dunia ambalo sasa limebakiza mwaka mmoja tu kuanza kutimua vumbi.

“Hatutapanic lakini tunajua tunahitaji kuwa bora. Kuna mawazo mapya, kuna wachezaji wapya wanakuja kwenye timu ambao hawana uzoefu na michezo ya kimataifa. Ni mchanganyiko wa mambo mengi lakini sio kisingizio. Tunahitaji kujitafuta haraka, Kombe la Dunia liko karibu kwa hiyo kila kambi ni muhimu sana kwa sasa.” Aliongeza.

Baada ya kijipapatua kwa ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Andora jumamosi England walionesha kiwango nduni katika mchezo dhidi ya Senegal na hata mabadiliko 10 ya Tuchel hayakuwa na athari yeyote kwani Senegal walipata ushindi waliostahili baada ya Ismaila Sarr, Habib Diarra na Cheikh Sabaly kuhakikishia ushindi kwa Simba wa Terang’a.

Tuchel, Kocha wa zamani wa Chelsea, Bayern Munich na Paris Saint-Germain aliajiriwa na jukumu la kubwa la kuipeleka England hatua moja mbele kuelekea kwenye michuano mikubwa ya ulaya baada ya kupoteza katika fainali mbili zilizopita. Hata hivyo England bado wako katika nafasi nzuri ya Kwenda Marekani mwakani baada ya kushinda mechi zote tatu za kufuzu kwa kombe hilo hadi sasa dhidi ya Albania, Latvia na Andorra.

Related Articles

Back to top button