Yanga yajipanga kwa Makubwa Ligi ya Mabingwa Afrika

DAR ES SALAAM: KATIKA hali inayoonesha dhamira ya dhati ya kujiongeza kimataifa, msemaji wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe, amesema matokeo ya msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika yamekuwa funzo muhimu kwa klabu hiyo.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya msimu ujao, Kamwe amesema timu imejifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza msimu huu na sasa inalenga hatua kubwa zaidi kama robo fainali, nusu fainali au hata kucheza fainali ya mashindano hayo.
Kamwe amebainisha kuwa Yanga imeonesha ubora mkubwa kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kufanikiwa kushiriki michuno ya kimataifa huku ikiwa imebakiza mechi tano mkononi. linawapa nafasi ya kujipanga mapema kwa safari ya kimataifa.
“Msimu ujao tunaenda Ligi ya Mabingwa tukiwa na kumbukumbu isiyo nzuri ya kuishia hatua ya makundi msimu huu. Kila mwanayanga anatamani kuona timu yake ikirudi kwenye mafanikio ya kufika robo, nusu au hata fainali kama ilivyokuwa kwa baadhi ya timu zilizofanikiwa zaidi,” amesema Kamwe.
Katika maandalizi hayo, Kamwe amefafanua kuwa benchi la ufundi linaendelea na kazi ya kuandaa ripoti mahsusi itakayowasaidia kubaini wachezaji wa kuongeza nguvu kwenye kikosi. Lengo ni kuwa na kikosi imara kitakachoweza kupambana na wapinzani wa kiwango cha juu barani Afrika.
Kamwe ametolea mfano wa timu ya Pyramids kutoka Misri amesema kuwa wamekuwa somo kwa Yanga. “Pyramids wametufundisha kuwa si lazima uwe umeshiriki michuano hiyo kwa miaka mingi ili ufanikiwe, bali kufanya usajili sahihi na kuwa na mipango bora ya kiufundi kunaweza kukuwezesha kushindana,” amesema.
Yanga imejipanga upya na kwa ari mpya kuelekea msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa na nia ya kulinda heshima ya klabu na taifa kwa ujumla kupitia mafanikio ya kimataifa.