Madrid yampa miaka 6 Trent

MADRID:MABINGWA wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa barani ulaya, Real Madrid wametangaza kumsajili Beki wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya England Trent Alexander-Arnold kwa mkataba wa miaka sita baada ya zaidi ya miaka 20 Liverpool, na kuongeza kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 atacheza Kombe la Dunia la Klabu.
Real madrid ilimsajili Alexander-Arnold kabla ya mkataba wake kumalizika, na hivyo kumfanya apatikane kukiwasha kwenye Kombe la Dunia la Klabu nchini Marekani litakaloanza kuumiza nyasi Juni 14 hadi Julai 13 mwaka huu.
Katika taarifa ya kuthibitisha usajili huo Liverpool imesema itakuwa ikipokea kiasi cha fedha kwa huduma za beki huyo machachari akiwa Bernabeu kwa huduma yake, na dili lake litakamilika mara tu dirisha litakapofunguliwa jumapili ya Juni 1. Alexander-Arnold anaondoka Liverpool FC bila kinyongo akiwaacha mashabiki na mioyo ya shukrani kwa mchango wake klabuni hapo.
Alexander-Arnold, ambaye ameichezea Liverpool mechi 354 tangu alipocheza mechi yake ya kwanza kwenye timu ya wakubwa mwaka 2016, alitangaza mapema mwezi huu ataondoka katika klabu hiyo aliyojiunga nayo akiwa na umri wa miaka sita, huku mkataba wake ukitarajiwa kumalizika Juni 30 mwaka huu.
Akiwa Liverpool Trent ametwaa mataji 8 yakiwemo Ligi Kuu nchini England, UEFA Champions League, UEFA Super Cup, FIFA Club World Cup, FA Cup, Carabao Cup Pamoja na Ngao ya jamii. Trent anaungana na swahiba wake mkubwa Jude Bellingham katika viunga vya Santiago Bernabeu