Ligi Kuu

Nafasi ya tatu yainyima usingizi Azam FC

DAR ES SALAAM: WAKATI pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara likiwa limefungwa kwa muda, hali ni tofauti kabisa ndani ya kikosi cha Azam FC, hawana muda wa kupumzika, wakihaha kuhakikisha wanamaliza msimu huu wakiwa katika nafasi ya tatu.

Kwa sasa, Azam FC inashikilia nafasi ya 3 wakiwa na alama 57 baada ya michezo 28, nyuma ya Simba SC yenye alama 69 (michezo 26) na vinara Yanga waliokusanya pointi 73 kwenye michezo 27. Licha ya tofauti hiyo ya alama, Azam FC wanang’ang’ania kulinda nafasi yao ya tatu kwa nguvu zote.

Kwa mujibu wa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Zakaria Thabiti ‘Zaka’, wachezaji wa Azam hawajapewa mapumziko kipindi hiki cha mapumziko ya ligi. Badala yake, wameendelea na mazoezi chini ya Kocha Rachid Taoussi, wakijiandaa vilivyo kwa michezo miwili iliyosalia.

“Tunaendelea na mazoezi kila siku, wachezaji wanatokea nyumbani na kufika Azam Complex kwa ajili ya mazoezi. Pia tumecheza mechi kadhaa za kirafiki, ikiwemo dhidi ya timu yetu ya vijana, ili kuwapa nafasi wachezaji kuendelea kuwa fiti,” amesema Zaka.

Azam FC imepanga kutumia michezo hiyo miwili ya mwisho kama fursa ya kuthibitisha ubora wao na kumaliza msimu kwa heshima. Wanatarajiwa kuikaribisha Tabora United kwenye dimba lao la Azam Complex kabla ya kukamilisha msimu kwa safari ya kwenda Babati, kuwavaa Fountain Gate FC katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa.

Licha ya malengo ya awali kuwa kumaliza nafasi mbili za juu kutofikiwa, Azam FC wanatambua umuhimu wa kuhitimisha msimu wakiwa na heshima, na zaidi kujiandaa kwa msimu ujao kwa morali ya ushindi.

Related Articles

Back to top button