Msanii Jux azindua EP yake

DAR ES SALAAM:MSANII maarufu wa Bongo Fleva, Juma Mkambala almaarufu Jux, ameendelea kuwasha moto wa mapenzi kwa kuachia rasmi EP yake mpya “A Day To Remember”, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya ndoa yake na mrembo Priscy.
Baada ya kuibua gumzo na sherehe sita za kifahari nchini Nigeria, Jux atahitimisha safari ya harusi Mei 28 katika ukumbi wa Super Dome, Masaki, Tanzania.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Jux amesema kazi hiyo ni zaidi ya muziki — ni simulizi ya upendo wao, inayochora picha ya safari yao ya mahaba, urithi wa kitamaduni na furaha kama wanandoa.
EP hiyo ina vibao vilivyoshirikisha wakali kama Phyno kutoka Nigeria na D Voice kutoka Tanzania, ikiunganisha sauti na ladha za Afrika Mashariki na Magharibi.
Watayarishaji waliotengeneza kazi hiyo ni pamoja na S2kizzy, Foxx Made It, na Aykbeats, huku Lizer Classic akisuka mixing na mastering kwa ustadi wa hali ya juu.
Katika ujumbe wake, Jux alimshukuru mke wake, familia, timu nzima na mashabiki waliomuunga mkono. Ameahidi pia kuachia wimbo maalum mara baada ya harusi ya Dar es Salaam kama zawadi ya kufunga ukurasa huu muhimu wa maisha yake.
EP “A Day To Remember” itapatikana kwenye majukwaa yote ya kusikiliza muziki kuanzia usiku wa leo.
Jux, ambaye kwa sasa anatikisa na wimbo wa “Sijui Anadate na X wa Nani Lakini Anampenda”, anatarajiwa kufunika kila sherehe ya awali kupitia tukio hilo kubwa la mwisho nchini Tanzania.