
SINGIDA: KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma, amesema ingawa timu yake imefanikiwa kupata tiketi ya kushiriki Michuano ya Afrika (CAF), bado wana kazi kubwa ya kufanya katika michezo mitatu iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ouma ameweka wazi kuwa lengo lao kwa sasa ni kuhakikisha wanamaliza ligi wakiwa katika nafasi ya tatu, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Azam FC.
Singida Black Stars, kwa sasa wanashika nafasi ya nne kwa alama 53 baada ya michezo 27, wanapambana kusogea mbele zaidi. Azam FC wako nafasi ya tatu kwa alama 57 baada ya michezo 28, pengo hilo linaonekana kuwa dogo na linaweza kufutwa kama Singida wataendelea na ushupavu waliouonesha msimu huu.
Ratiba iliyobaki kwa Singida Black Stars si rahisi. Watakutana na Simba SC na Dodoma Jiji FC wakiwa ugenini, kabla ya kukamilisha msimu kwa mchezo wa nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons.
“Jambo la kujivunia ni kwamba tumepata tiketi ya kucheza michuano ya Afrika, akili yetu sasa ni kuhakikisha tunamaliza ligi kwa heshima na kuonesha kuwa tuna uwezo wa kushindana katika michuano hiyo mikubwa,” amesema.
Ouma ameongeza kuwa mafanikio ya kufuzu CAF yamewapa motisha zaidi na timu yake ipo tayari kujituma hadi mwisho wa msimu huu ili kujiandaa kwa changamoto mpya zinazowasubiri barani Afrika.